IKISIRI
Matini yoyote ya fasihi huhitaji kusomwa na kueleweka ili ipate kuwa na maana. Hata hivyo, maana ya matini hujitokeza ikiwa msomaji ataelewa mtindo uliotumika kuisuka. Japo huu ndio ukweli, mapitio tangulizi ya maandishi yameonyesha kuwa kuna tafiti chache zilizofanywa kwa kina katika kubainisha mtindo katika fasihi kama kipengele muhimu na kinachojisimamia kufafanua maana na hasa katika tamthilia za Arege. Hivyo basi utafiti huu umehakiki mtindo uliotumika katika tamthilia tatu za Arege ili kutoa mchango katika kuzielewa tamthilia hizi kwa kina. Ili kufikia lengo kuu, tumechanganua, vipengele mbalimbali vya kimtindo ili kuonyesha umaarufu wao katika uwasilishaji wa maudhui tukiongozwa na maswali matatu ambayo ni: i) Arege ametumia mbinu gani za usimulizi kuwasilisha maudhui katika tamthilia teule? ii) Mbinu za usimulizi alizotumia zimesaidia vipi uwasilishaji wa maudhui katika tamthila teule? iii) Je, tamathali zilizotumika zimesaidia vipi kuwasilisha ujumbe katika tamthilia teule? Utafiti umeongozwa na nadharia ya Uhakiki wa Kimtindo iliyoasisiwa na Leech. Kimsingi, nadharia hii hujihusisha na uchunguzi wa jinsi lugha inavyotumika ili kuleta ujumi katika matini za fasihi. Katika kuchunguza mtindo, ndipo usanii wa kazi ya fasihi hutambulika na kuelezea nafasi ya mwandishi katika kuimulika jamii katika uhalisia wake. Matini za Arege zilizohakikiwa kimtindo ni tamthilia tatu ambazo ni: Kijiba cha Moyo, Mstahiki Meya na Chamchela. Mbinu ya kimaksudi ya kuteua sampuli ndiyo ilitumika katika kuchagua tamthilia teule tatu ili kuwakilisha uandishi wa Arege katika kipengele cha mtindo. Data ya utafiti ilipatikana maktabani kutokana na usomaji wa maandishi yaliyohusiana na malengo na maswali ya utafiti. Uchanganuzi wa data uliongozwa na mbinu ya uhakiki matini ambapo data iliyokusanywa ilipangwa kwa kuegemea maswali ya utafiti ambapo vipengele vya kisintaksia na kisemantiki katika tamthlia zilizoteuliwa vilibainiswa na kuchambuliwa. Data iliyopatikana ilipangwa kwa kuzingatia malengo ya utafiti na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo ya kinathari. Utafiti huu umebaini kwamba mtindo ndio huamua jinsi ujumbe unavyopokelewa na unavyoeleweka. Vilevile, imegunduliwa kwamba Arege ametumia lugha kwa ubunifu na hivyo kuleta ujumi katika maudhui anayosuka katika tamthilia zilizoteuliwa. Aidha, utafiti umebaini kuwa Arege ametumia mtindo wa kinaya ili kuwakejeli Waafrika waliouandama ukoloni mamboleo kikasuku. Mtindo huu umetawala katika tamthilia zote ili kuonyesha kuwa lengo la Arege ni kuwaonyesha Waafrika kuwa wao ndio chanzo cha shida wanazokumbana nazo. Utafiti huu ni wa manufaa kwa wasomi na wapenzi wa fasihi kwa kuwa umetoa mwanga wa kuzielewa na kuzielezea tamthilia tatu zilizoteuliwa kimtindo. Kwa waandishi wa fasihi, utafiti unawafaa kwani utawawezesha kuelewa mbinu mbalimbali za kuandika matini zenye mvuto wa kisanaa ili kuwasilishia jamii ujumbe kwa ubunifu mkubwa. Aidha, utafiti ni wa manufaa kwa watafiti kwani watakapousoma watakuwa katika nafasi bora ya kuuwekea wao msingi.
Oiko, F (2021). Uhakiki Wa Mtindo Katika Tamthilia Za Arege. Afribary. Retrieved from https://afribary.com/works/uhakiki-wa-mtindo-katika-tamthilia-za-arege
Oiko, Fridah "Uhakiki Wa Mtindo Katika Tamthilia Za Arege" Afribary. Afribary, 08 May. 2021, https://afribary.com/works/uhakiki-wa-mtindo-katika-tamthilia-za-arege. Accessed 18 Dec. 2024.
Oiko, Fridah . "Uhakiki Wa Mtindo Katika Tamthilia Za Arege". Afribary, Afribary, 08 May. 2021. Web. 18 Dec. 2024. < https://afribary.com/works/uhakiki-wa-mtindo-katika-tamthilia-za-arege >.
Oiko, Fridah . "Uhakiki Wa Mtindo Katika Tamthilia Za Arege" Afribary (2021). Accessed December 18, 2024. https://afribary.com/works/uhakiki-wa-mtindo-katika-tamthilia-za-arege