Asili Ya Wapemba Kwa Mtazamo Wa Isimu Mandhari

IKISIRI

Tasnifu inahusu uchunguzi juu ya Asili ya Wapemba kwa Mtazamo wa tawi la Isimujamii la Isimu Mandhari. Isimu Mandhari ni mkabala wa kiisimu unaoshughulikia vipashio vya lugha vinavyohusiana na eneo fulani la watumiaji wa lugha inayohusika. Huchunguza umaeneo ndani ya lugha fulani. Kwa mfano, kuchunguza msamiati wa lugha unaotumika katika eneo fulani. Kipashio kimojawapo cha lugha, yaani maneno ya kategoria ya nomino (majina) yanachukua nafasi kubwa katika mkabala huu. Majina yanatuwezesha kupambanua maeneo mbalimbali ya watumiaji wa lugha inayohusika. Majina yana taarifa nyingi ziwahusuzo watumiaji wa majina hayo. Majina huakisi mfumo wa maisha ya jamii inayohusika. Ni sehemu ya kipashio cha lugha kinachopokea mabadiliko ya haraka kulingana na maendeleo yanayofikiwa katika jamii. Hivyo, majina yanaweza kutumika katika kuchunguza asili na historia ya watumiaji wa majina hayo. Kazi hii ilitumia majina ya watu na majina ya maeneo katika kisiwa cha Pemba kuchunguza asili ya Wapemba.

Wanaisimujamii wanaamini kuwa utambulisho wa mtu unaweza kubainika kutokana na vigezo anuai vinavyoonekana na visivyoonekana. Massamba na wenziwe (2009:46) wamemnukuu Tabouret-Keller (1989), wameeleza kuwa utambulisho wa mtu umefungamana na mambo mengi ya kijamii kama vile lugha, utamaduni, mila na desturi, mavazi, chakula, dini (imani mbalimbali), historia ya jamii, siasa na uchumi. Kigezo cha mahali alikozaliwa mzungumzaji kinapaswa kuzingatiwa wakati wa utambulisho. Matumizi ya majina ya familia, majina ya vitu na majina ya matukio yamebainishwa na Massamba na wenziwe (2009:52-56) kuwa ni vibainishi vya utambulisho wa mtu na jamii kwa ujumla. Buberwa (2011) amechunguza

mofolojia (muundo) wa majina ya vituo vya daladala jijini Dar es Salaam kama sehemu ya majina mahususi ambayo haijashughulikiwa kwa nadharia za kimuundo. Miongoni mwa wataalamu waliobainishwa na Buberwa (2011) kuwa wamechunguza vipengele anuai kuhusu majina ni Allen (1945), Powicke (1954), Roden (1974), Brown (1975), Schotsman (2003), Angus (2005), Rugemalira (2005), Rye (2006), Majapelo (2009) na Rayburn (2010). Okal (2012) ameonesha jinsi majina ya watu yalivyowashughulisha baadhi ya watafiti. Imeelezwa kuwa majina huwa na dhima muhimu katika jamii.

Data nyingi zilikusanywa uwandani. Maeneo tofauti ya kisiwa cha Pemba yalihusishwa. Mbinu ya awali tuliyoitumia katika ukusanyaji wa data ilikuwa ni ugawaji wa madodoso kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari za Pemba ili kutusaidia katika kuyatambua maeneo ya awali kukaliwa pamoja na maeneo yenye taarifa za kihistoria. Baadaye, mbinu ya mahojiano ilitumika. Ushuhudiaji pamoja na uzoefu wetu kwa maeneo ya utafiti viliturahisishia zoezi la ukusanyaji data na udhibiti wake. Mbinu ya udurusu wa maandiko ilitusaidia wakati wa kusoma kazi za waandishi mbalimbali. Data zilichambuliwa kwa mbinu ya maelezo kwa mwongozo wa nadharia ya Onomastiki.

Uchunguzi wetu ulibaini kuwa majina yatumiwayo na Wapemba kama utambulisho wa mtu binafsi, ukoo wake au eneo analoishi yana taarifa nyingi kuhusu jamii inayohusika. Taarifa tulizozikusudia sisi ni zile zilizotuwezesha kufahamu asili ya jamii hiyo. Kupitia majina ya watu na majina ya maeneo tulibaini kuwa Wapemba ni watu wenye asili mchanganyiko baina ya Waafrika kutoka bara (Tanzania) na Waarabu (Washirazi) kutoka bara Arabu. Umuhimu wa matokeo ya utafiti huu unadhihirika kutokana na kuweka wazi hoja zilizoshindwa kupata mwafaka miongoni mwa watafiti waliotangulia kuhusu asili ya Wapemba. Tunaamini kuwa hitimisho la utafiti huu linakidhi mahitaji ya kitaaluma juu ya dhana iliyochunguzwa kwani taarifa zilizoelezwa humu zinahalisika.

Overall Rating

0

5 Star
(0)
4 Star
(0)
3 Star
(0)
2 Star
(0)
1 Star
(0)
APA

Hamad, A (2021). Asili Ya Wapemba Kwa Mtazamo Wa Isimu Mandhari. Afribary. Retrieved from https://afribary.com/works/asili-ya-wapemba-kwa-mtazamo-wa-isimu-mandhari

MLA 8th

Hamad, Abdallah "Asili Ya Wapemba Kwa Mtazamo Wa Isimu Mandhari" Afribary. Afribary, 26 Apr. 2021, https://afribary.com/works/asili-ya-wapemba-kwa-mtazamo-wa-isimu-mandhari. Accessed 30 Nov. 2024.

MLA7

Hamad, Abdallah . "Asili Ya Wapemba Kwa Mtazamo Wa Isimu Mandhari". Afribary, Afribary, 26 Apr. 2021. Web. 30 Nov. 2024. < https://afribary.com/works/asili-ya-wapemba-kwa-mtazamo-wa-isimu-mandhari >.

Chicago

Hamad, Abdallah . "Asili Ya Wapemba Kwa Mtazamo Wa Isimu Mandhari" Afribary (2021). Accessed November 30, 2024. https://afribary.com/works/asili-ya-wapemba-kwa-mtazamo-wa-isimu-mandhari